Watu wengi huwa wanatamani kudumu kwenye uhusiano lakini bahati mbaya huwa inashindikana.
Mtu ambaye hadumu kwenye uhusiano, si kwamba anakuwa anapenda, bali inatokea tu kutokana na sababu mbalimbali.
Labda, huenda pengine ni kutokana na tabia zake au za mwenzake. Mfano, yawezekana akawa anaongea ‘mdomo’ sana, yawezekana akawa mbinafsi. Au ana hulka ya ugomvi lakini mwenzake hana. Yawezekana akawa na tabia za kuchepuka na mfano wa hizo.
Lakini inawezekana tatizo likawa la mwenzake, Akawa ana tabia zisizompendeza mpenzi wake. Kama ubinafsi, hasira kali au akawa na tabia mbaya ambazo mwenzake ameshindwa kuzivumilia.
Kikubwa tu, watu hushindwa kudumu penzini kwa kupishana mambo mbalimbali. Kuanzia tabia, mtindo wa maisha na wengine kutoelewana dhumuni la safari yao.
Mara kadhaa nimekuwa nikisisitiza, unapoanzisha uhusiano na mwenzako lazima kwanza mjue lengo au madhumuni ya huo uhusiano wenu. Mwanamke ajue kwamba uhusiano wao ni wa muda mrefu au wa muda mfupi.
Una malengo au hauna? Vivyo hivyo mwanaume, kwa kinywa chake, kutoka moyoni athibitishe lengo na madhumuni ya uhusiano wake ili mwenzake ajue kabisa kwamba yupo kwenye uhusiano wa aina gani. Baada ya hapo ndio muanze safari.
Na hii ndio siri ya maisha. Ndiyo siri ya uhusiano wote. Mkishajua madhumuni ya safari yenu, kinachofauta ni kukipa umuhimu kipaumbele chenu. Pamoja na kujua kwamba mtakumbana na changamoto mbalimbali katika safari yenu lakini mnapokumbuka umuhimu wa safari yenu, mnatiana moyo. Mnapokutana na magumu yasiyokuwa na mfano, hamkati tamaa. Mnainuka na kusimama tena. Kila mmoja anapomuona mwenzake kakosea, anambebea makosa yake na kumsamehe kulingana na uzito wa safari yao.
- Kusikilizana ndio jambo kubwa sana katika safari yenu. Asiwepo mtu wa kumdharau mwenzake. Mwanamke, amthamini mwenzi wake kuliko mtu mwingine yeyote. Mwanaume, amthamini mwanamke wake katika kiwango cha hali ya juu. Asikubali kuyumbishwa na tamaa za kimwili, asirudishwe nyuma na maneno ya watu na kisiwepo kizingiti chochote cha kumkatisha tamaa.Kwa vyovyote itakavyokuwa, suala lenu la ‘utaifa wa uhusiano’ ndio mlitangulize mbele. Muishi mkijua kwamba, uhai wa penzi lenu mmeushikilia nyinyi wawili. Mna kila sababu ya kulilinda penzi lenu kwa gharama yoyote kwani mafanikio ya uhusiano wenu, ni mafanikio ya wote wawili.
- Mpendane. Mheshimiane katika kiwango cha juu. Kila mmoja atambue majukumu yake. Mwanamke amtii mwanaume, amheshimu. Mwanaume ampende sana mwanamke. Asimdharau, atambue thamani yake katika nyumba licha ya kwamba mwanaume ndio kichwa cha familia.
- Mwanaume asivimbe kichwa. Amshirikishe mwenzake katika masuala yanayohusu maisha na uhusiano wao. Hata ikitokea mmepishana kauli, shukeni. Kila mmoja aongozwe na busara kwamba, ipo njia mbadala ya kuwavusha kwenye mabishano hayo bila kusababisha mtafaruku.
- Mwanamke usiwe mzungumzaji sana kwa mwanaume. Mpe faraja pale inapobidi. Farijianeni katika vipindi mbalimbali mnavyopitia. Muanguke na kuinuka pamoja. Asiwepo mmoja kati yenu achukulie changamoto ya mwenzake kama si yake.
- Kila mmoja aguswe na matatizo ya mwenzake. Mnapokuwa kwenye furaha, kwa pamoja pia mfurahi. Msiwe na tamaa. Tengenezeni maisha yenu mnayoyataka. Kwa pamoja mtakuja kufurahia ushindi wa safari yenu.
0 Comments